KAIMU KAMISHNA WA UHIFADHI TAWA AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MENEJIMENTI YA TAWA

Na. Mwandishi wetu, Mwanza.



Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Mlage Yussuf Kabange amefungua rasmi kikao kazi cha Menejimenti ya TAWA kilichofanyika Disemba 13,2025, katika ukumbi wa Malaika, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho kilichojumuisha Makamishna Wasaidizi Waandamizi, Makamanda wa Kanda na Wakuu wa Vituo vyote vya TAWA, Kamishna Kabange amesema lengo kubwa la kikao hiki ni kuboresha utendaji kazi ili kufikia malengo ya Mamlaka.



Kamishna Kabange ameibainisha kuwa kikao kazi hiki kitajikita katika vipaumbele mbalimbali vitakavyoboresha maeneo ya utendaji kazi wa TAWA yakiwemo maeneo ya ulinzi na usimamizi wa wanyamapori, ukusanyaji wa mapato, migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ujenzi wa miundombinu katika hifadhi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi hususan kwenye maeneo ambako askari wanafanya kazi.

Sambamba na hilo, Kamishna Kabange amewasisitiza Makamishna Wasaidizi Waandamizi na Makamanda wa Kanda kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu unazingatia utu, sheria na haki bila upendeleo wowote.




Awali, akimkaribisha Kamishna wa Uhifadhi, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Kurugenzi ya Huduma za Shirika, Maarufu Thabit Mkwaya amesema katika kikao kazi hiki viongozi wa Menejimenti watapata fursa ya kupitishwa katika mawasilisho mbalimbali yanayolenga kujenga uwezo wa kiutendaji, kuongeza ubunifu, kujitathmini, kubadili mitazamo na fikira za viongozi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Kamishna Maarufu ameongeza kuwa miongoni mwa mawasilisho hayo ni tathmini ya mpango mkakati wa Mamlaka (2021/22-2025/26) na maandalizi ya mpango mkakati mpya (2026/27-2030/31), Uongozi wa Kimkakati na Akili Hisia, Itifaki na Adili kwa viongozi, Afya ya Akili pamoja na Elimu ya Fedha na Uwekezaji.














Comments

Popular posts from this blog

KUNDI LINGINE LA WANANCHI 541 LAHAMA NGORONGORO

𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 “𝐒𝐄𝐑𝐄𝐍𝐆𝐄𝐓𝐈 𝐍𝐀𝐓𝐈𝐎𝐍𝐀𝐋 𝐏𝐀𝐑𝐊 𝐆𝐎𝐋𝐅 𝐂𝐎𝐔𝐑𝐒𝐄” 𝐖𝐀𝐅𝐈𝐊𝐈𝐀 𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐌𝐈𝐀 𝟒𝟐

UTALII WA MALIKALE WASHIKA KASI NCHINI, WAFARANSA WAFURIKA KILWA KISIWANI